02/07/2018

VODACOM TANZANIA FOUNDATION PAMOJA NA CHUO KIKUU HURIA WAENDESHA SEMINA YA USAWA JINSIA SHINYANGA


Vodacom Tanzania Foundation, taasisi isiyo ya kiserikali ya ushirikiano na jamii ya Vodacom Tanzania Plc, leo imefanya semina ya usawa wa jinsia wilayani Shinyanga. Semina hiyo iliyoandaliwa kwa kushirikiana na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania imefanyika mjini Shinyanga na inalenga kutoa elimu ya maswala ya jinsia kwa washiriki 105.
Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kina jukumu la kuanzisha na kutekeleza sera ya jinsia inayoendana na makubaliano ya kitaifa na kimataifa ili kujenga usawa wa kijinsia na uwezeshwaji wanawake chuoni hapo na katika jamii ya Tanzania kwa ujumla. Kwa sababu hii, Chuo hicho kimeandaa mpango wa uelimishaji juu ya maswala ya jinsia kwenye shule za sekondari na vyuo, pamoja na vyuo vikuu wilayani Shinyanga kwa kushirikiana na taasisi ya Vodacom Tanzania Foundation. Walengwa wa semina hii ni wanafunzi na waalimu kujadili maswala ya jinsia na uelewa katika jamii, jambo ambalo inategemewa litasaidia upatikanaji wa elimu mkoani Shinyanga.


Pamoja na kuridhia mikataba ya kimataifa na sera zake, utekelezaji umekuwa mdogo kutokana na mapungufu katika mfumo wa sheria na uelewa mdogo katika jamii, jambo ambalo limepelekea Wanawake kubaniwa haki zao. Wanawake bado wanakosa haki zao za kibinadamu, hawashirikishwi kwenye maamuzi yanayowaathiri wala kupata uwakilishi unaotosha, wanakumbana na ubaguzi kwenye ajira, wananyimwa kumiliki ardhi na mali na hukumbana na ukatili majumbani mwao au katika jamii. Changamoto nyingine ni pale ambapo wasichana wanazuiwa kuhudhuria shule au kupata huduma za afya. Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) madhara ya ukatili huu yanakuwa makubwa siyo tu kisaikolojia na kimwili bali pia familia na jamii nzima huathirika, jambo linalodumaza maendeleo ya taifa kiuchumi.


Akiongelea sababu za Vodacom kuhusika na mpango huu wakati wa ufunguzi wa semina hii, George Venant, Mkuu wa kanda ya Tanganyika wa Vodacom Tanzania, alisema, “Vodacom Tanzania Foundation ilianzishwa kwa lengo la kuwezesha wanawake na wasichana nchini Tanzania kupata elimu bora, kuweza kufikia na kupata huduma bora za afya na pia kuwawezesha kuanzisha na kuendeleza biashara zao kwa nia ya kuwaimarisha kiuchumi ili waweze kutimiza malengo yao ya maisha. Tulifanya hivi kwa kuona kiasi gani wanawake na wasichana wamekosa ushirikishwaji katika ngazi mbali mbali kwenye jamii zetu.”


Katika ufunguzi wa semina hiyo, mgeni wa heshima alikuwa Mkuu wa Mkoa wa 
Shinyanga, Mh.Zainab Telak, ambaye alielezea uhitaji wa mabadiliko katika elimu kwa wasichana mkoani humo akisema, “Tunashukuru taasisi hizi kuamua kushirikiana na kuleta semina hii hapa Shinyanga, haswa kipindi hiki ambapo kuna uhitaji mkubwa. Takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 70 ya wasichana wanafeli mitihani ya darasa la saba, kiwango ambacho ni juu sana kulinganisha na maeneo mengine ya Tanzania.”
Mkuu wa Vodacom Tanzania kanda ya Tanganyika alizungumzia ushirikiano na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania katika kuandaa semina hii, “Hata hivyo, tunaelewa vizuri sana kuwa msaada mkubwa zaidi kwa wanawake na wasichana nchini ni kuwawezesha wajitatulie shida zao wenyewe na kuweza kukwepa vipingamizi kwa malengo yao. Njia kuu ya kufanya hivi ni kuwaelimisha wanawake wenyewe pamoja na jamii zao. Kwa hiyo basi, tunafurahi sana kushirikiana na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kuleta semina hii hapa Shinyanga. Chuo Kikuu Huria cha Tanzania ni taasisi ambayo ina historia ndefu ya kutoa elimu ya kiwango cha juu nchini na kwa njia ambazo zinawawezesha Watanzania wengi zaidi kuifikia. Na, kwa sera ilizojiwekea, iko mstari wa mbele kuhakikisha kuwa inatoa elimu kwa kuzingatia haki na usawa kijinsia na wamefanikiwa kuhitimisha idadi kubwa na ya kuheshimika ya wanafunzi wa kike.”
‘Tumejiwekea lengo la kusaidia vijana nchini kujitambua na kuwezeshwa kutawala maisha yao na ndoto zao. Tatizo la kunyimwa haki kwa wanawake na wasichana ni pingamizi moja kubwa sana kwa uwezo wa vijana kujiendeleza kiuchumi na hata kisaikolojia.” Alisema Venant.
Semina hiyo inategemewa kujenga uelewa wa maswala ya jinsia katika jamii ya Shinyanga na hivyo kuleta mabadiliko kwa wanafunzi wa kike mkoani humo. Venant alimalizia kwa kusema, “Katika mafanikio tunayotegemea nyinyi washiriki kuondoka nayo ni pamoja na uelewa kamili wa maswala ya jinsia na kuongezeka hali ya kujiamini kwenu, jambo ambalo litasaidia upatikanaji wa elimu hapa Shinyanga na pia mtaweza kuwaelimisha wazazi na walezi ili, kwa pamoja, tuweze kuleta mabadiliko yanayohitajika katika jamii yetu.”

Kuhusu Vodacom Tanzania Foundation
Vodacom Tanzania Foundation inawasaidia wanawake na wasichana nchini kuboresha afya yao, kujipatia elimu bora na kujenga biashara mpya. Kwa ushirikiano na taasisi zisizo za kiserikali nchini na wadau, Vodacom Tanzania Foundation imesaidia miradi zaidi ya 120 mpaka sasa na kuwekeza zaidi ya Shilingi bilioni 15 katika jitihada za kuboresha maisha ya Watanzania.
Kwa maelezo zaidi tafadhali tembelea www.vodacom.co.tz

Kuhusu Chuo Kikuu huria cha Tanzania
Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kinatoa kozi za shahada na nyingine kwa bei nafuu, ubora na ubunifu. Vile vile chuo kinahakiksha mazingira yanayowezesha mafunzo endelevu kwa wanafunzi, wafanyakazi na waalimu wake.
Chuo kimeandaa na kinaedneleza maqzingira bora ya kuendeshea utafiti na kutoa machapisho. Inachapisha matokea ya tafiti zake ikiwa ni sehemu ya kujenga, kuhifadhi na kusambaza uelewa katika machapisho yake yenyewe na mengine ya kitaifa na kimataifa.
Huduma kwa jamii ni jambo liliwekwa wazi katika majukumu ya Chuo. Pia, Chuo kinashirki shughuli mabali mbali za kijamii ikiwa sehemu ya ushirikiano na jamii.
Kwa maelezo zaidi tembelea: www.out.ac.tz

Copyright © 2018 Vodacom Tanzania. All Rights Reserved.