05/07/2018

VODACOM TANZANIA YATANGAZA AWAMU YA PILI YA TUSUA MAPENE

 

Kampuni ya mawasiliano ya simu inayoongoza nchini, Vodacom Tanzania, leo imetangaza awamu ya pili ya mchezo wa ‘TUSUA MAPENE’ baada ya kumalizika kwa awamu ya kwanza na mshindi mkuu kupatikana.

Awamu ya pili ya TUSUA MAPENE inaongeza njia za ushiriki pamoja na idadi ya zawadi zitakazoshindaniwa. Kuanzia sasa, mchezo utakuwa wazi kwa watumiaji wa mitandao yote ya simu nchini kupitia M-PESA Wakala.

Akiongea na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Mkurugenzi wa Kitengo cha Biashara cha Vodacom Tanzania, Hisham Hendi amesema, “Awamu ya kwanza ya Tusua Mapene imemalizika kwa kishindo baada ya mshindi mkuu wa zawadi ya Shilingi milioni 290 kupatikana. Hata hivyo, bado kuna shauku kubwa miongoni mwa wateja wetu na Watanzania wengi kuendelea na mchezo huu. Sasa tumeona ni vema basi tutoe nafasi kwa Watanzania wengi zaidi kupata nafasi ya kushinda zawadi hizi. Kwa kuwa mfumo wetu wa M-PESA sasa umeunganishwa na mitandao mingine yote nchini, basi uwezo huo sasa tunao.”

Awamu ya kwanza ya TUSUA MAPENE ilianza tarehe 14 Agosti mwaka 2017 na kumalizika tarehe 30 Juni mwaka 2018. Zaidi ya Shilingi bilioni 1.7 zimetolewa kama zawadi katika kipindi cha miezi kumi iliyopita kwa washindi 326, wakiwemo wawili walioshinda shilingi milioni 100 kila mmoja na washindi wengine 323 wa zawadi za kila siku na kila mwezi. Na hatimaye alipatikana mshindi wa zawadi kuu ya awamu ya kwanza aliyejishindia Shilingi 290,409,580/- .

Kwenye mkutano huo na waandishi wa habari, mshindi mkuu wa awamu ya kwanza bw. Jackson Andrew Mwankema kutoka Tukuyu-Mbeya alisema, “Nilikuwa na imani na mchezo huu muda wote kwa sababu niliona Vodacom wakitangaza washindi mara kwa mara lakini sikutegemea kushinda mwenyewe zawadi kuu hii. Kwa kweli nimeona kama ndoto hivi maana sasa mambo mengi ambayo nimetamani kufanya kwa ajili yangu na familia pamoja na jamii sasa nitaweza.”

Katika awamu ya pili, zawadi zimeongezwa ili kuongeza nafasi za ushindi na hivyo idadi ya washindi kila siku, kila wiki na kila mwezi. Bw. Hendi alifafanua zaidi, “Tutakuwa na mashindano ya kila siku, kila mwezi na michezo mikuu bila mabadiliko makubwa. Katika awamu hii, mshindi ataarifiwa kuwa ameshinda nafasi ya kucheza ‘Gurudumu la Bahati’ kuona zawadi atakayopata. Vile vile, kuongeza idadi ya washindi, tumeanzisha zawadi ndogo ndogo za papo hapo, ili kuongeza fursa za ushiriki.”

Washiriki wa TUSUA MAPENE awamu ya pili watakuwa na nafasi ya kujishindia zawadi za kila siku kati ya Shilingi laki moja hadi milioni 40 kutegemeana na jinsi mshiriki alivyocheza, na zawadi za kila mwezi kati ya Shilingi laki tatu na milioni 30. Zawadi kuu zitaanzia Shilingi milioni 5 hadi zawadi kuu ya awamu ya pili ambayo itakuwa inaongezeka kadri mchezo unavyoendelea. Vile vile, kutakuwa na zawadi za papo hapo zitakazoshindaniwa kila siku ambapo mshindi mmoja anaweza kushinda milioni 100 na wengine 20 wanaweza kushinda Shilingi milioni 20.

Bw. Hendi alimalizia kwa kusema, “Vodacom Tanzania tunaendeleza historia yetu ya ubunifu na ubora wa huduma kwa wateja wetu pamoja na kujali matakwa yao. Kuboresha na kupanua ushiriki wa TUSUA MAPENE ni jambo moja tu, na tunategemea kupata washindi zaidi ya laki tatu na arobaini kwa mwaka 2018/19. Kwa hiyo Watanzania kaeni tayari KUTUSUA MAPENE na kubadilisha maisha yenu.”

 

 

Kuhusu Vodacom Tanzania Plc

Vodacom Tanzania PLC ni kampuni ya mawasiliano inayoongoza ikiwa na mtandao wa data wenye kasi zaidi nchini. Tunawapatia huduma ya mawasiliano wateja zaidi ya milioni 12. Vodacom Tanzania na kampuni zake tanzu ni sehemu ya Vodacom Group iliyosajiliwa nchini Afrika Kusini ambay na yenyewe inamilikiwa na Vodacom Group Plc ya uingereza. Imesajiliwa kwenye Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) ikiwa na namba ya usajili ISIN:TZ1886102715 na jina: VODA.

Copyright © 2018 Vodacom Tanzania. All Rights Reserved.