12/07/2018

VODACOM TANZANIA FOUNDATION YAIPIGA TAFU PAUKWA CHILDREN’S FESTIVAL

Kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom Tanzania Plc kupitia taasisi yake ya shughuli za kijamii ya Vodacom Tanzania Foundation imeshirikiana na Ngoma Afrika Performing Arts Company na kudhamini Paukwa Children Arts Festival, katika kutoa hamasa ya kutunza mazingira pamoja na tamasha la ngoma za kitamaduni ambazo hushirikisha wanafunzi mbali mbali wa Manispaa ya Morogoro.

Paukwa Children Arts Festival hufanyika kila mwaka ikiwa na lengo la kuwapa watoto fursa ya kuonyesha uwezo wao wa kutunga na kucheza ngoma za kitamaduni. Vile vile huwapa watoto nafasi ya kujitambua, kuburudika na kupata maarifa mapya kutokana na kukutana na walimu na watu wa aina mbali mbali ambao hutoa elimu ya ziada wakati wa ngoma hizo.

Akizungumza mjini Morogoro wakati wa tukio hilo, Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano wa Vodacom, Bi. Jacquiline Materu alisema kuwa Vodacom inatambua na kuthamini mchango wa watoto kwenye Taifa hili. “Tunaelewa na kutambua umuhimu wa Paukwa Children Arts Festival na ndio maana tumeamua kuungana pamoja kwa mwaka huu. Paukwa Children Arts Festival imekuwa ikifanyika kila mwaka na ni ukweli kwamba imechangia na kuwapa nafasi watoto kutambua uwezo wao. Ni matumaini yangu kuwa ngoma hizi zitazidi kuimarisha tamaduni zetu kama Watanzania,” alisema Bi. Jacquiline.

Bi. Jacquiline aliongeza kuwa kwa mwaka huu kutakuwa na shughuli mbali mbali za kijamii ambazo zitazidi kuweka Paukwa Children Arts Festival karibu. Alizitaja shughuli hizo kama kununua mbegu za miti ya maembe, kupanda miti aina ya maembe, kutambulisha kwa watoto jinsi ya kutunza taka taka na kuwa na mazingira masafi, kununua vitunzia taka – (waste bins) pamoja na kununua vinywaji kwa watoto.

“Moja kati ya jambo muhimu ambalo serikali imekuwa ikiipa kipaumbele ni pamoja na utunzaji wa mazingira na upandaji wa miti ili kuendana na mabadiliko ya hali ya hewa. Sisi Vodacom Tanzania tumeona ni vema tushiriki na hawa watoto kwenye upandaji wa miti aina ya miembe. Nina imani kuwa hawa watoto wataweza kutambua umuhimu wa utunzaji wa mazingira na hapo mbeleni tutakuwa na mazingira safi kwani wataendeleza huo utamaduni,” aliendelea kufafanua Mkuu huyo wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano.

Vile vile, kutakuwa na warsha kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa waalimu wa muziki. Hii pia itaenda sambamba na wafanyakazi wa kampuni ya Vodacom kujumuika pamoja na washiriki wa Paukwa Children Arts Festival hali ambayo itasababisha watoto kujisikia furaha na amani. Hii itazidi kuwajengea uwezo wa kutunga na pia kutambua uwezo walionao katika kuendeleza Sanaa hapa nchini, aliongeza Bi. Jacquiline.

Kwa upande wake, Mkuu wa wilaya ya Morogoro Bi Regina Chonjo ambaye alikuwa mgeni rasmi alisema kuwa Paukwa Children Arts Festival inalengo la kutoa hamasa na msisimko kwa muziki na ngoma za kitamaduni, kuonyesha uwezo wa kutunga, uwezo wa kujieleza na kutambua jukumu la muziki kwenye kukuza elimu ya mtoto. Hii ni moja ya maeneo ambayo taasisi ya Vodacom Tanzania Foundation imekuwa ikiunga mkono kwani pia inachangia ukuaji watoto huku wakiwa na uwezo wa kutambua na kutumia vipaji vyao.

Paukwa Children Arts Festival huandaliwa na kuendeshwa na kampuni ya Ngoma Afrika Performing Arts kwa kushirikiana na Manispaa ya Morogoro pamoja na wadau wengine wanaojitokeza. Wazo hili lilitokana na mradi wa majaribio wa Children as Creators (CAC) ambao uliendeshwa na Manispaa ya Morogoro kwa kushirikiana na  Ngoma Afrika chini ya ufadhili wa ubalozi wa Denmark - the Royal Danish embassy kupitia shirika la  Danish Centre for Culture and Development (DCCD), alisema Chonjo huku akiipongeza Taasisi ya Vodacom Tanzania Foundation kwa kudhamini Paukwa Children Arts Festival.

Vodacom Tanzania Foundation inawasaidia wanawake na wasichana nchini kuboresha afya yao, kujipatia elimu bora na kujenga biashara mpya. Kwa ushirikiano na taasisi zisizo za kiserikali pamoja na wadau nchini, Vodacom Tanzania Foundation imesaidia miradi zaidi ya 120 mpaka sasa na kuwekeza zaidi ya Shilingi bilioni 15 katika jitihada za kuboresha maisha ya Watanzania.

Kwa maelezo zaidi tafadhali tembelea:

Vodacom Tanzania PLC ni kampuni ya mawasiliano inayoongoza ikiwa na mtandao wa data wenye kasi zaidi nchini. Tunawapatia huduma ya mawasiliano wateja zaidi ya milioni 12. Vodacom Tanzania na kampuni zake tanzu ni sehemu ya Vodacom Group iliyosajiliwa nchini Afrika Kusini ambayo na yenyewe inamilikiwa na Vodacom Group Plc ya uingereza. Imesajiliwa kwenye Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) ikiwa na namba ya usajili ISIN:TZ1886102715 na jina: VODA.

Copyright © 2018 Vodacom Tanzania. All Rights Reserved.