02/06/2020

Kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom Tanzania PLC kwa kushirikiana na Global Publishers leo wamezindua huduma mpya ijulikanayo kama ‘HADITHI ZA SHIGONGO’ ambayo itapatikana kupitia kipengele cha VODACOM HADITHI kupitia namba 0901767676. Vodacom hadithi imekuwa ikiwapa burudani wateja wa Vodacom tangu mwaka 2018.

“Tukitambua umuhimu wa huduma zetu kumfikia mteja kiganjani kupitia maendeleo ya kidijitali, Vodacom tumeungana na mtunzi mahiri wa riwaya mbalimbali za kusisimua na kuelimisha, ndugu Eric Shigongo na tunakuletea wewe mteja wetu wa Vodacom hadithi mbalimbali kutoka kwa mtunzi huyu kupitia huduma hii mpya ya hadithi za Shigongo,” alisema Mkurugenzi wa huduma za Kidijitali bwana Nguvu Kamando.

Kamando aliongeza, "tunaamini muungano huu kati ya Vodacom, Global Publishers na kampuni ya teknohama ya Premier Mobile Solutions, utaleta huduma bora kabisa kwa mteja wa Vodacom, tukianza na hadithi na simulizi mbalimbali na baadaye tutakuwa na huduma nyingine za kuelimisha na kuburudisha jamii kwa ujumla”.

Akiongea kwa niaba ya Global Publishers, Meneja Mkuu wa Global Publishers, bwana Abdallah Mrisho alisema, “tunaamini ubunifu huu mahiri kutoka kwa Vodacom Tanzania wa kuweza kuhamisha riwaya mbalimbali za vitabu kuwa katika mfumo wa sauti, utasaidia kuwafikia wateja wengi wa Vodacom nchini, wateja hawa walikuwa na kiu ya kusoma hadithi za Shigongo kwa siku nyingi, lakini sasa wanaweza kusikiliza hadithi hizi kutoka kwenye simu zao za mkononi”.

Akifafanua zaidi kuhusu huduma hii mpya, Kamando alisema kwamba huduma hii imetengenezwa mahususi kwa kuzingatia hali ya kipato cha mtanzania. Mteja wa Vodacom ana uwezo wa kujiunga kwa siku au wiki au kununua kifurushi cha kusikiliza hadithi zote zinazopatikana katika huduma hii ya VODACOM HADITHI.

Kuhusu kujiunga na huduma hii, bw. Kamando alisema, "mteja wa Vodacom anaweza kujiunga kwa njia mbili, ya kwanza ni kwa kupiga namba 0901767676 na kufuata maelekezo au njia ya pili mteja anaweza kutuma neno SHIGONGO kwenda namba 15460. Mteja akishajiunga atapokea ujumbe wa uthibitisho na kulipia Tsh 100/= kwa siku kwa huduma ya SIKU, Tsh 450/= kwa huduma ya WIKI au Tsh 1000/= kwa huduma ya mwezi” na kisha kujulishwa jinsi ya kusikiliza Hadithi yake.

Bw Kamando aliongeza kwamba huduma hii itamwezesha mteja wa Vodacom kujitoa muda wowote atakapojisikia na anaweza kurudi tena na kufurahia huduma ya Vodacom Hadithi pale atakapohitaji tena. Iwapo mteja atapata changamoto yoyote, atatuma neno MSAADA kwenda namba 15460 na tatizo lake litatatuliwa,.

Kuhusu kusitisha huduma hii, bw. Kamando alieleza kwamba mteja anayetaka kusitisha huduma, atatuma neno ONDOA au ACHA kwenda namba 15460 na huduma hii itasitishwa papo hapo.

Aidha, Vodacom inatoa OFA kwa wateja wake wa mwanzo ya kusikiliza hadithi za Shigongo bure kabisa kwa siku mbili za mwanzo.

Copyright © 2020 Vodacom Tanzania. All Rights Reserved.