28/02/2019

Vodacom yarahisisha VICOBA kuweka akiba kidijitali

Katika jitihada za kurahisisha shughuli za vikundi vidogo vya kutunza akiba, Vodacom Tanzania PLC kwa kushirikiana na Benki ya TPB leo wamezindua huduma ya kwanza na ya kipekee nchini kwa ajili ya vikundi vya kuweka akiba vilivyo rasmi (VICOBA) na visivyo rasmi iitwayo M-Koba.  

Huduma hii mpya ya M-Pesa itawezesha vikundi kutunza fedha kidijitali, kwa usalama na uwazi zaidi. Suluhisho hili linalenga kusaidia mahitaji ya vikundi rasmi vya kuweka akiba na mikopo (VICOBA, VSLAs, CB) pamoja na vikundi mbali mbali visivyo rasmi.

Inakadiriwa kuwa asilimia 16 ya watanzania (zaidi ya watu milioni 4.4), wengi wao wakiwa wanawake, ni wanachama wa vikundi zaidi ya 50,000 vya kuweka akiba na mikopo (VICOBA) ambao huhifadhi akiba zaidi ya TZS bilioni 100 kwa mwaka. Mbali na vikundi hivyo rasmi, kuna idadi ya zaidi ya vikundi 50,000 visivyo rasmi ambavyo vinaweka akiba na kutoa mikopo kupitia mitandao ya vikundi vya wahitimu, vyama vya kifamilia, vikundi vya watu wanaofanya kazi sehemu moja na kadhalika.

 Akizungumza wakati wa uzinduzi wa huduma hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Bw. Hisham Hendi alisema "huduma hii ya kidijitali inalenga kutoa huduma endelevu ambayo itatumiwa na kufikia vikundi vilivyopo maeneo mbalimbali nchini kwa njia ya mtandao mkubwa wa Vodacom".

Aliongeza kwamba Vodacom imedhamiria kufikia idadi kubwa ya watu ambao hawapo kwenye mifumo rasmi ya kifedha, kuchochea ujumuishwaji, na uwezeshaji kupitia huduma hii rafiki, salama na yenye uwazi wa hali ya juu.

Huduma hii itaongeza angalau moja ya tatu ya idadi ya watu waliosajiliwa katika mifumo rasmi ya kifedha, na zaidi kufikia wanawake wa vijijini, ambao ndio asilimia kubwa zaidi ya idadi hiyo. “Kama taasisi ya kifedha, tunatambua umuhimu wa vikundi hivi na ndio sababu tumeshirikiana na vinara hawa wa sekta ya simu kuleta suluhisho hili la kidigitali ambalo litarahisisha kutunza akiba na kuwezesha watu kufikia malengo yao" alisema Afia Mtendaji Mkuu wa TPB Bw. Sabasaba Moshingi.

"Tunashukuru kuwa Vodacom na TPB wamekuja na huduma mpya ambayo imetatua matatizo tuliyokuwa nayo. Sasa tuna mfumo salama zaidi wa vikundi vyetu na tunachanga kwa uwazi kwani mfumo huu unaruhusu kuonekana kwa shughuli za kikundi" alisema Abdallah Mkenga, mwenyekiti wa kikundi kimojawapo cha Vicoba aliyehudhuria hafla ya uzinduzi.

Kwa kuimarisha shughuli za vikundi vya akiba kidijitali zaidi, huduma hii itatengeneza mazingira wezeshi ambayo yatakuza utamaduni wa kuweka akiba, usimamizi imara wa kifedha na kukuza ujumuishwaji wa fedha nchini kwa njia ya M-Pesa.

Mwisho…

Hakimiliki © 2018 Vodacom Tanzania. Haki zote zimehifadhiwa