30/12/2019

Ikiwa miezi mitatu imepita tangu Kampuni ya Vodacom Tanzania Plc kutoa gawio la Sh. bilioni 50.4 kwa wanahisa wake, Kampuni hiyo leo inatangaza kutoa riba ya ziada kwa watumiaji wake wa huduma za kifedha kupitia simu ya mkononi. Zaidi ya wateja milioni 8.3 wa Vodacom M-Pesa watapata sehemu yao ya faida ya bilioni 9 iliyokusanywa kwenye akaunti ya M-Pesa Trust kama faida ya kutumia huduma hiyo kwa kipindi cha mwezi Aprili hadi Septemba.

Mkurugenzi wa Vodacom Tanzania M-Commerce, Epimack Mbeteni, alisema kuwa, faida hiyo italipwa kwa wateja wote ikiwamo wakala wa rejareja na washirika wengine wa M-Pesa ambapo faida yao italipwa kulingana na jinsi walivyofanya miamala ya malipo kupitia M-Pesa.

“Huduma yetu ya pesa kupitia simu ya mkononi kwa maana ya M-Pesa, inaendelea kuleta simulizi zenye mafanikio, ikitoa dhamana muhimu za kijamii na thamani ya kifedha kwa watanzania wote. Tumeshuhudia ukuaji katika jukwaa la watumiaji wa M-Pesa, ambapo zaidi ya wateja, mawakala, wafanyabiashara wakubwa na taasisi watapata gawio hili.  Tunafurahia kuona ongezeko hilo kwa wateja wetu wanaotumia huduma ya M-Pesa,” alisema

Kwa mujibu wa Takwimu za hivi karibuni kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Vodacom Tanzania PLC, kampuni inayoongoza kwa mawasiliano ya simu nchini ina wateja zaidi ya milioni 10 kwenye jukwaa lake la M-Pesa ikiwa ni asilimia 41 katika mgawanyiko wa umiliki wa soko. Hadi sasa Vodacom Tanzania PLC imekwishalipa riba ya zaidi ya shilingi bilioni 130 kwa wateja wake wa M-Pesa.

Epimack aliongeza kwa kusema kuwa, sehemu ya faida kwa wateja huhesabiwa kulingana na mwongozo wa Benki Kuu ya Tanzania na itategemea kiwango cha shughuli za M-Pesa zilizofanywa kwa kipindi husika.

“Mgao huo ulianza tangu wiki ya kwanza ya sikukuu ambapo mteja anatuma ujumbe mfupi wa neno AMOUNT kwenda 15300 ili kufahamu kiasi cha faida ya riba atakachopokea. Baada ya kupokea kiasi hicho kilichotolewa, wateja wa M-Pesa wanaweza kutoa riba zao kupitia pesa taslimu, muda wa maongezi au vifurushi, na kulipa bili au kulipia bidhaa mbalimbali ” alisema.

Jukwaa la Vodacom M-Pesa linaongoza kwa kutoa fursa kwenye soko ambapo limeongeza kasi katika ujumuishaji wa kifedha na kuchochea shughuli za uchumi nchini Tanzania.

“Kwa kipindi cha miaka 11 iliyopita tumejitahidi kuwekeza zaidi kwenye uvumbuzi ambapo kupitia ushirikiano wetu wa kimkakati na benki pamoja na wavumbuzi wengine, tumeenda mbali zaidi ya kufanya miamala kwa kuanzisha bidhaa nyingine kama M-Koba, M-Pawa, Halal Pesa, Songesha, M-Pesa MasterCard na nyinginezo nyingi. Tunaendelea kuhakikisha tunakuza ujumuishaji wa kifedha na kukuza uchumi wa kidijitali nchini Tanzania,” Alielezea Mbeteni.

 

Kuhusu Vodacom M-Pesa Tanzania:

Vodacom M-Pesa ni huduma ya kifedha kwa njia ya simu inayoongoza nchini iliyoanzishwa na Vodacom Tanzania PLC mwaka 2008. Kwa sasa ni moja ya huduma chache duniani zilizopewa tuzo ya ubora ya GSMA na ina wateja zaidi ya milioni 10. Kwa kiasi kikubwa M-Pesa imechangia katika kukua kwa huduma za kifedha na shughuli za uchumi nchini. Wateja wanatuma na kuweka pesa kupitia huduma ya M-Pesa kupitia kwa mawakala zaidi ya 106,000 nchini kote. Mfumo wa M-Pesa unaunganisha mabenki, makampuni na mashirika ya Serikali katika kufanya malipo ya kidigitali.

Kwa sasa, M-Pesa inaendelea kuwa kinara katika soko la huduma za kifedha nchini kupitia huduma zake za kibunifu kama vile Akiba na Mikopo, malipo ya kieletroniki, huduma za vikundi na nyingine nyingi ambazo zinakidhi mahitaji ya watanzania na kuwezesha ufikaji na utumiaji Zaidi wa huduma rasmi za kifedha.

Hakimiliki © 2020 Vodacom Tanzania. Haki zote zimehifadhiwa