VPL Updates

Morrison Amfunika Tena Kagere

BERNARD Morrison siyo mtu mzuri kabisa, hivyo ndivyo unavyoweza kusema. Achana na lile bao aliloifunga Simba katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa Jumapili iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa, Dar.

Imebainika kuwa mchezaji huyo wa kutumainiwa wa Yanga anavaa kiatu cha kuchezea soka cha bei mbaya kushinda cha staa wa Simba, Mnyarwanda, Meddie Kagere.

Katika uchunguzi ambao umefanywa na Championi Jumatatu, limebaini kuwa kiatu alichovaa Morrison katika mchezo huo kilikuwa na thamani ya dola 300 (sawa na Sh 685,785) ambacho ni Adidas Predator 20+FG, Black/Red.

Wakati huo Kagere katika mchezo huo alikuwa amevalia kiatu aina ya Puma Futere Netfit 19.3 FG/AG, Red ambacho thamani yake ni dola 98.99 (sawa na Sh 226,286).

Hata hivyo, Morrison ameliambia Championi Jumatatu kuwa ubora wa kiatu hicho pia ulichangia kupiga faulo safi iliyomshinda kipa wa Simba, Aishi Manula na kutinga wavuni.

“Ninamshukuru Mungu lakini pia na mke wangu kwa zawadi ya kiatu kwani yeye ndiye aliyekuja nacho.

“Hata hivyo, sijui kama mimi ndiye nina kiatu cha thamani zaidi ya wengine lakini naamini wapo wachezaji ambao wanavaa viatu vya bei mbaya zaidi kushinda mimi,” alisema Morrison.

Hakimiliki © 2020 Vodacom Tanzania. Haki zote zimehifadhiwa